1232 22nd St. NW Washington D.C 20037
ubalozi@tanzaniaembassy-us.org
202-939-6125 202-884-1080 202-884-1083 (Visa)
Embassy of Tanzania, DC

Hotuba ya Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB.), Waziri Mkuu Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wakati Wa Ufunguzi wa Kongamano la Jumuiya ya Watanzania Nchini Marekani – Tarehe 31 Agosti, 2018

MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mhe. Issa Haji Ussi Gavu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar;

Mhe. Balozi Wilson Masilingi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani;

Mhe. John Chelminiak, Meya wa jiji la Bellevue;

Mhe. Salum Maulid Salum, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar;

Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

Waheshimiwa Mabalozi;

Wawakilishi kutoka Serikali ya Marekani na Tanzania;

Bw. Lunda Asmani, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya DICOTA;

Bw. Charles Bishota, Rais wa (DICOTA);

Washiriki na Wageni wote waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

HABARI ZA ASUBUHI,

Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo katika Kongamano hili la Watanzania wanaoishi Marekani (DICOTA).

Napenda pia kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa DICOTA kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika Kongamano hili ambapo kwa hakika limeandaliwa kwa ustadi mkubwa kama ilivyo desturi yenu.

Aidha, niupongeze Ubalozi wetu hapa Marekani kwa kuendelea kushirikiana na uongozi wa DICOTA tangu kuanzishwa kwa makongamano haya. Hakika makongamano haya yamekuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake. Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha mnachangia vilivyo kwenye maendeleo ya nchi na hatimaye Tanzania iweze kufikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Hongereni sana!

KAULIMBIU YA KONGAMANO LENU LA MWAKA HUU

Mabibi na Mabwana,

Nawapongeza kwa kuchagua Kaulimbiu sahihi kuongoza Kongamano lenu: Ushiriki wa Wanadiaspora katika Uwekezaji, Ubunifu na Viwanda. Sambamba na hilo, niwapongeze kwa upangaji mzuri wa mada na wawasilishaji wake. Vilevie, nimevutiwa na uwepo wa washiriki mahiri katika mijadala yote. Wakati napitia mada na ratiba yenu, nilifurahishwa sana na namna zilivyopangiliwa kwa kuzingatia masuala muhimu yanayoigusa jamii yetu kama vile afya, elimu, masuala ya viwanda, uwekezaji na mengineyo.

Kwa ujumla wake, mada hizi zimebebwa na Kaulimbiu inayotia hamasa: Ushiriki wa Wanadiaspora katika Uwekezaji, Ubunifu na Viwanda. Niwapongeze tena kwa kauli mbiu hii ambayo inahamasisha juhudi za kuleta maendeleo nchini. Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza na kuhimiza uwekezaji, ubunifu na uanzishwaji wa viwanda nchini ili kuleta maendeleo chanya na kuifanya nchi kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa msingi huo, tunapoona mnachagua kauli mbiu yenye kuendana na mipango iliyopo ya Serikali; kwa kweli tunafarijika sana. Ni rai yetu kuwa muendelee kuwa moja wa wadau muhimu wa kuleta maendeleo yenye tija kwa taifa lenu la asili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

JUHUDI ZA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Mabibi na Mabwana,

Kabla sijahitimisha maelezo yangu haya, naomba nitumie fursa hii kueleza japo kwa uchache masuala mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikiyasimamia:-

Hali ya Amani na Utulivu Kiuchumi

Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa hali ya amani nchini inakuwa nzuri ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kuendesha shughuli zao za kiuchumi na maendeleo. Hilo linadhihirishwa na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watalii, wafanyabiashara na wawekezaji nchini. Ripoti ya pamoja iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Benki Kuu (BOT) , Kitengo cha Taifa cha Takwimu (National Bureau of Statistics – NBS ) – Idara ya Uhamiaji na Tume ya Utalii ya Zanzibar ( Zanzibar Commission of Tourism – ZCT ), inaonesha kuwa idadi ya watalii waliongia Tanzania kwa mwaka 2016 ni 1,284,279 ukilinganisha na mwaka 2015 ambao ni watalii 1,137,156. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 12. Mwaka 2017 watalii waliongezeka pia na kufikia watalii 1,327,143.

Aidha ripoti hiyo inaonesha mapato yanayotokana na Sekta ya Utalii yamekuwa yakiongezeka kila mwaka. Kipindi cha mwaka 2016 mapato yanayotokana na utalii yalifikia dola za Kimarekani bilioni 2.1, ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo mapato yalikuwa dola za Kimarekani bilioni 1.9 . Mwaka 2017 mapato yanayotokana na Utalii yalifika dola za Kimarekani bilioni 2.3 .

Ajira na Elimu

Kwa upande wa ajira na elimu, Serikali imekuwa ikitangaza nafasi za ajira mara kwa mara, ambazo nyingine zilitokana na nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliondolewa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa sifa na wengine kuwa watumishi hewa. Serikali inaendelea kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu hususan kujenga na kukarabati madarasa na ofisi za walimu na kuongeza madawati.

Vilevile, Serikali imefuta michango yote iliyokuwa mzigo kwa wazazi. Hivi sasa, kila mwezi Serikali inapeleka jumla ya shilingi bilioni 20.8 kwenye Shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Elimumsingi bila Malipo. Kwa upande wa elimu ya juu na vyuo vikuu; Serikali inapeleka mikopo ya wanafunzi kwa wakati. Katika mwaka wa masomo 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 427.55 zimetumika kama mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu wapatao 122,623.

Nitumie nafasi hii kuwapongeza baadhi ya Diaspora ambao wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali katika sekta ya elimu na afya. Kipekee, niwapongeze wale Wanadiaspora ambao walinufaika na Mikopo ya Elimu ya juu na sasa wanachukua hatua za makusudi kurejesha mikopo hiyo. Hongereni sana kwani mikopo hiyo mnayorejesha ni muhimu sana ili kutoa fursa kwa Watanzania wengine kunufaika nayo.

Uimarishaji Uchumi

Serikali imeweka mkazo mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ili kuweza kupata fedha za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kuwaletea maendeleo Watanzania. Wote ni mashahidi jinsi ukusanyaji wa mapato ulivyoongezeka ambapo kwa sasa kiasi cha wastani wa shilingi trillion moja na nukta tatu hukusanywa kwa mwezi. Tumepata mafanikio haya kutokana na Serikali kupitia na kuhakiki orodha ya watu wanaostahili kulipa kodi na serikali inahakikisha wanalipa kodi stahiki.

Kwa upande wa jitihada za kukuza uchumi, Serikali inafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufufua viwanda vilivyokuwa havifanyi kazi na vilevile kujenga na kuimarisha miundombinu mbalimbali hasa ile ya usafiri. Mathalan, kuanza ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa yaani Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora, Dodoma umbali wa kilometa 722 ambapo takriban shilingi trilioni 7.062 zitatumika. Baadaye tutaunganisha na Mwanza, Kigoma na nchi za jirani. Kukamilika kwa reli hiyo kutaongeza mahusiano ya kibiashara na majirani zetu wa Rwanda, Uganda,Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na matokeo chanya kwenye ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo.

Kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha viwanja vyake ikiwemo Dar es Salaam (Terminal III), Kilimanjaro, upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza ili kiwe na hadhi ya kimataifa, upanuzi mwingine unaoendelea katika viwanja vya Mtwara, Tabora, Kagera na Kigoma. Bila shaka mmeshuhudia dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano kufufua Shirika letu la ndege ATCL. Mwezi Julai mwaka huu tumepokea ndege ya Kwanza aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyoruka toka hapa Seattle na kwenda moja kwa moja hadi Dar es Salaam bila kutua popote. Ndege tatu aina ya Bombardier zilitangulia. Nyingine mbili kubwa aina ya Bombardier zinatarajiwa mwaka huu. Mwaka kesho 2019 tunapokea ndege ya pili aina ya Boeing 787-8 Dreamliner. Shabaha ni kuanza safari za moja kwa moja toka Marekani, Ulaya na Asia hadi Dar es Salaam, Zanzibar na Kilimanjaro, ili kuongeza idadi ya Watalii.

Eneo lingine muhimu la kiuchumi ni upatikanaji wa nishati ya kutosha na uhakika. Katika kuhakikisha kunakuwepo na nishati ya kutosha kwa ajili ya kuunga mkono falsafa ya uchumi wa viwanda, Serikali inatekeleza mradi mkubwa kabisa wa umeme wa waji wa Rufiji (maarufu kama Stiegler’s Gorge) utakaozalisha MW 2,100 utakapokamilika.

Marekani inaongoza kwa kuleta watalii wengi Tanzania. Mwaka 2015 Marekani ilileta watalii 66,394; mwaka 2016 watalii 86,860 na mwaka 2017 watalii 87,238. Nchi inayofuatia kwa kuleta watalii wengi Tanzania ni Uingereza. Utalii unachangia asilimia 17 ya pato la Taifa (GDP) na kutengeneza ajira zaidi ya milioni 1.5. Uchumi unakua kwa wastani wa asilimia 7; Mfumuko wa bei uko chini ya asilimia 3.3 July 2018 ( The lowest since series began in 1999); akiba ya fedha za kigeni inatosha kuagiza bidhaa nje ya nchi kwa miezi mitano.

Serikali inaamini kuwa uwepo wa amani na utulivu ndiyo msingi wa kufikiwa kwa ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye pato la kati linaloongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Serikali inaendelea kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili bila ubaguzi wowote kama vile rangi, kabila au tofauti za kiitikadi. Serikali imeendelea kushughulikia changamoto ya ukosefu wa ajira, kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za nchi, kupambana vikali na rushwa na uhujumu uchumi kwa kusimamia misingi ya uadilifu, weledi na uaminifu katika utumishi wa umma.

DIASPORA KUMBUKENI KUWEKEZA NYUMBANI

Mabibi na Mabwana,

Mtakubaliana nami kuwa nchi nyingi duniani hususan za Bara la Asia na baadhi barani kwetu Afrika zimekuwa zikinufaika sana na mchango wa Diaspora wake. Hivyo, nitumie fursa hii kuwataka muendelee kutumia taaluma zenu mnazozipata huku na rasilimali mbalimbali kusaidia maendeleo nyumbani. Siku zote muwe ni wenye kujivunia na kukumbuka nyumbani. Kumbukeni nyumbani ili mpafanye napo panoge kama huku mnapokimbilia!

Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itazidi kupiga hatua kimaendeleo na kupata utaalam wa kutosha katika nyanja mbalimbali. Bado kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu ili kuendeleza maeneo mapya ya kiuchumi yanayoibuka na yale yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano.

Tunahitaji wahandisi kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kuimarisha sekta ya mafuta na gesi na utekelezaji wa mipango miji. Vilevile, tunahitaji madaktari kwa ajili ya kuendeleza hospitali zetu na wahadhiri katika vyuo vikuu ili kukuza Sekta ya Elimu ambayo ndio msingi katika kujenga sekta nyingine. Sina shaka kwamba fursa hizi mtazichangamkia na mtakuwa tayari kuja nyumbani kufanya kazi katika sekta hizo.

MWISHO

Mabibi na Mabwana,

Naomba sasa kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru tena waandaaji kwa kunialika. Nitoe rai kwa Diaspora wote wa Kitanzania popote mlipo kujivunia nchi yenu na kuona fahari kuitwa Watanzania kwani nchi yetu inafahamika na kuheshimika sana duniani.

Aidha, nawaombeni kuendelea kutafuta na kushawishi wawekezaji katika sekta za Viwanda, Utalii, Elimu, Afya, Kilimo na Mawasiliano ili waje kuwekeza kwa wingi nyumbani. Serikali yenu itaendelea na jukumu lake la msingi la kuandaa mazingira wezeshi kwa Diaspora na wageni kwa lengo la kuwahamasisha na kuwashirikisha katika kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini.

Baada ya kusema haya, naomba kutamka kuwa Kongamano la Jumuiya ya Watanzania Wanaoishi Nchini Marekani (DICOTA) kwa mwaka 2018 sasa limefunguliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!